Search This Blog

Saturday, 14 January 2017

JPM alivyokoshwa na ‘Wilaya Moja, Bidhaa Moja’

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/3517814/highRes/1535185/-/maxw/600/-/wpje7r/-/

By Faustine Fabian, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Bariadi. Ziara ya Rais John Magufuli mkoani Simiyu imeendelea kuwa gumzo kutokana na maagizo mbalimbali aliyoyatoa mkoani humo.
Hata hivyo, kiongozi huyo ambaye alimaliza ziara hiyo siku tatu zilizopita anakumbukwa kwa kuelezea kufurahishwa na mkakati wa uongozi wa mkoa huo kuanzisha mradi wa uzalishaji mali kila wilaya kupitia kaulimbiu ya ‘Wilaya Moja, Bidhaa Moja.’
Magufuli alisema mpango huo siyo tu utaongeza uzalishaji, bali pia utawahakikishia soko la ndani na nje ya mkoa wazalishaji,  hivyo kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na mkoa kwa jumla.
Alitoa pongezi alipohutubia mikutano ya hadhara katika miji ya Bariadi na Maswa akiwa ziarani mkoani Simiyu mwanzoni mwa wiki.
Rais Magufuli alisema wakuu wengine wa mikoa wanapaswa kujifunza kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka namna ya kutumia fursa na rasilimali zinazopatikana maeneo yao kuinua uchumi wa wananchi.
Awali, Mtaka alisema wamejipanga kutekeleza kwa vitendo sera na ahadi ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda vinavyotumia malighafi inayopatikana maeneo hayo ikiwamo ngozi, maziwa na pamba.
Mtaka alisema tayari kimeanzishwa kiwanda cha chaki wilayani  Maswa na cha maziwa wilayani Meatu. Vingine vitakavyoanzishwa na wilaya husika kwenye mabano ni cha  ngozi na pamba (Bariadi), maji ya dripu (Busega) na cha sabuni (Itilima).
“Ni mkakati wetu kuwa Mkoa wa Simiyu ijitosheleze na kuuza nje mahitaji ya pamba za hospitali pamoja na bidhaa zingine zinazozalishwa na malighafi yanayopatikana mkoani mwetu,” alisema Mtaka akimweleza Rais Magufuli.
Pamoja na kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na ajira kwa vijana, mkakati huo pia unalenga kuufanya mkoa wa Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa itakayoongoza kuchangia zaidi  pato la taifa ifikapo mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment