Search This Blog

Tuesday, 31 January 2017

WANAUME WALALAMIKIWA UTUNZAJI WATOTO

Wanaume washitakiwa matunzo ya watoto

MALALAMIKO yanayohusu huduma za utunzaji wa watoto yameongezeka zaidi kwa mwaka 2016 kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikitajwa kuwa ni hali ya uchumi kubadilika nchini.

Kwa mwaka 2015, Mahakama ya Watoto Kisutu jijini Dar es Salaam, ilipokea malalamiko 17 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambao walipokea malalamiko yapatayo 154, hali ambayo si kawaida na miaka mingine.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto Kisutu, Devotha Kisoka katika wiki ya utoaji wa elimu na msaada wa sheria inayofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.

“Katika awamu hii ya tano ya serikali ya kubana matumizi malalamiko yamekuwa mengi sana kwani wanaume wengi ambao wana watoto wengi imewawia vigumu kuwatunza,” alisema Kisoka na kuongeza kuwa mashauri yanayohusu matunzo kwa watoto ni mengi, tangu ilipofutwa mianya ya ufisadi, wanawake wengi wameachwa na wamekuwa wakifika kwa kutokujua waende wapi na watoto.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanaume wengi wameamua kuelekeza fedha zao kutunza watoto wao wa ndani ya ndoa pekee na kuwapa kidogo wale walionao nje ya ndoa, jambo ambalo halikuwa hivyo kwa miaka ya nyuma.

Aidha, aliwahimiza wanaume kukumbuka wajibu wa kuwatunza watoto wao bila kujali hali yao ya kiuchumi wakitambua kuwa mtoto ana haki ya kulelewa na kupata matunzo.

Alisema sheria imewapa haki wazazi, walezi au yoyote mwenye maslahi ya mtoto kupeleka kesi katika Mahakama za Watoto kama kudai matunzo, mamlaka ya kisheria juu ya uangalizi wa mtoto na uasili wa kambo kwa kuwa mtoto ana haki ya kulelewa au kuwajua wazazi ama walezi.

Alisema kwa mwaka huu mashauri ya aina hiyo yameendelea kufika kwa wingi na kwa kuwa bado ni mapema, bado wataendelea kuyapokea.

Alisema asilimia kubwa ya wanaofika kufungua mashauri hayo ni wanawake wakidai kuachwa bila huduma kwa watoto, lakini pia hata wanaume hufika kwa madai ya kutaka kuruhusiwa kuwaona watoto ama kuwatembelea.

Kuhusu utendaji wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Watoto, Kisutu, Victoria Nongwa alisema hupokea mashauri mbalimbali yanayohusu watoto kwa kuwa nao hufanya makosa mbalimbali kama ilivyo kwa watu wazima.

Alisema mtoto ana haki ya kupata dhamana katika mashitaka yote isipokuwa yale ambayo sheria imetamka bayana hayana dhamana na wanaweza kupata adhabu kama amri ya kuachiwa kwa masharti kwa kipindi fulani lakini kisizidi miaka mitatu.

Alizitaja adhabu nyingine ni kulipa faini, adhabu ya kuripoti kwa ofisa ustawi wa jamii kwa kipindi fulani na adhabu ya kupelewa katika shule maalumu.

No comments:

Post a Comment