Mwaka mpya huooooo!! Umeishaingia mzima mzima na vijana tuliushangilia vilivyo ujio wa mwaka huu wa 2017, na wengine walidiriki hata kuukashifu mwaka uliopita kwa maneno ya kejeli.
Binafsi nasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, huenda kweli kijana mwenzangu wa siku hizi kuna mambo mengi yalikuendea ndivyo sivyo katika mwaka uliopita na kwa namna moja au nyingine ukashindwa kutimiza ndoto zako katika maisha.
Najua wapo vijana wa kike kwa kiume ambao mwaka 2016 mlipanga kufunga ndoa, kupata kazi, kujiunga na masomo ya elimu ya juu, kuanza biashara na wengine kujishughulisha na kilimo lakini kwa namna moja au nyingine hamkufanikiwa, lakini huu mwaka wa 2017 nao unaweza jipanga upya na kutazama wapi uliteleza na kushindwa kufikia malengo yako na kisha ukaanza upya harakati zako.
Ingawa wapo walioonesha bidii na kujituma katika kuhakikisha malengo yao yanatimia na mwisho wa siku yalikwama kwa sehemu ndogo aidha kwa kukosa mitaji au namna gani lakini sasa wanayo nafasi ya kuongeza bidii na kumalizia paliko baki.
Lakini pia katika kuhakikisha kuwa unatimiza ndoto au malengo yako mwaka huu 2017 na kuufanya kuwa mwaka wa historia kwako kijana, ni vyema ukajiweka pembembeni kabisa na makundi au magenge na mambo ambayo unadhani yalichangia sana wewe kurudi nyuma mwaka 2016.
Siku zote adui mkubwa wa kijana ni kijana mwenyewe! Unaweza kubisha lakini huo ndio ukweli. Leo hii kijana msomi ambaye wazazi walitumia gharama ya kukusomesha na wengine walipata mkopo wa kusoma lakini anaishia mtaani na kufanya vitu visivyo endana na taaluma aliyo nayo ni hasara.
Hebu epuka makundi ya vijana wenzako ambayo unadhani hayafuati maadili na hayafikirii maisha baada ya leo. Yes unawaza starehe kila kukicha na kuendekeza kupiga mizinga wenzako wanaofanya kazi si tabia nzuri.
Jipange kijana mwenzangu kabla hujapangwa na mzazi kibabe, mtoto wa kike unakaa kupiga rangi kucha nyumbani kila kitu unamuachia dada wa kazi, mwishowe hata ukipata mwenza wa kukuhamisha nyumbani mwaka huu unagwaya maana kila ukienda kwake we hata chai ya rangi mkanywe mgahawani maana huwezi kupika.
Vijana huu ni mwaka wa kazi kama anavyosema Rais John Magufuli kuwa tuchape kazi na maisha tutayaona mepesi tu tofauti na visingizio vya sasa.
No comments:
Post a Comment