Search This Blog

Sunday, 22 January 2017

Jinsi ya Kupunguza Uzito Kwa Njia za Asili: Njia 3 Rahisi

kupunguza-uzito-0

Uzito mkubwa wa kupindukia ni tatizo kubwa la kiafya katika maisha yetu ya kisasa. Uzito unapozidi kiwango ambacho kinahitajika kwa mtu husika kunachangia matatizo mengi ya kiafya. Watu wenye uzito mkubwa wamekuwa wakijaribu njia nyingi tofauti za kupunguza uzito bila ya mafanikio aidha kwasababu ya kukata tamaa mapema kabla ya matokeo au kwa kufuata njia zisizo sahihi na namna zisizo sahihi.
Baadhi ya matatizo yanayosababishwa na uzito mkubwa ni Kisukari ,Shinikizo la Juu la Damu na magonjwa mengine ya moyo.

Sababu za Kuongezeka Uzito wa Mwili:

Uzito mkubwa wa kupita kiasi unatokana na kuongezeka kwa mafuta mwilini ambayo hutunzwa sehemu mbalimbali mwilini kama juu ya ngozi,tumboni na juu ya viungo vya nadni vya miwili kama moyo,utumbo nk. Pia hujenga utando pembeni mwa mishipa ya damu.
Mafuta hutunzwa kama akiba pale mtu anapokula chakula kingi kuliko kiasi cha nguvu anazohitaji na hivyo mwili unabadilisha chakula hicho kuwa mafuta na kuweka katika akiba.
Watu wa mijini wananenepa zaidi kuliko wa vijijini kwasababu ya mitindo yetu ya maisha ambayo tunakula chakula kingi na chenye mafuta lakini hatuifanyishi miili yetu kazi za kutosha kutumia nguvu tulizoingiza.
Chukua mfano, mtu anakula kJ 5, mchana anakula kJ 20, jioni kJ 15 jumla ni Kj 40. Anaenda kazini kwa gari,anakaa masaa 8 kwenye kiti kazini kisha jioni anarudi na gari hadi nyumbani kwake. Umabali aliotembea ni mita 10-20 jumla ya nguvu ulizotumia jouli 30, nguvu zilizobaki bila matumizi ni kJ 10.
Sasa mwili unafanya nini na kJ 10 zilizobaki? Zinahifadhi kwa matumizi ya baadae kama mafuta ambayo hatakuja kuhitaji.
Fikiria inakuwaje katika siku 30 za mwezi na hifadhi hii. Hivi ndivyo uzito na unene unavyopatikana.
* kJ=Kilo Jouli (Kipimo cha nguvu mwilini)

Jinsi ya Kupunguza Uzito wa Mwili

  1. Kupunguza kiasi cha chakula kwa siku

kupunguza-uzito_ulaji-chakula
Hii ni njia moja kubwa ya kufanya usipate uzito mkubwa na pia kupunguza uzito.
Kama unahitaji kJ 30 kwa siku basi kama una uzito uliozidi utatakiwa kula kJ chache mfano kJ25 ili kJ 5 zinazohitajika zitoke katika akiba ya mafuta mwilini.
Uzito mkubwa unachangiwa kwa asilimia nyingi na kiasi kikubwa cha chakula mtu anachokula.
Naomba ifahamike kuwa suluhisho sio kuruka mlo,unatakiwa kula kila mlo ila kwa kiasi kidogo.
  1. Kufanya Mazoezi ya Mwili

kupunguza-uzito_mazoezi-2
Mazoezi ya mwili iwe kwa kufanya kazi au kwa kukimbia au katika vituo vya mazoezi au nyumbani yanasaidia kupunguza uzito kwa kuunguza mafuta ya akiba katika mwili. Mfano kama unakula kiasi unachohitaji tu kwa kazi za kawaida na kisha ukafanya mazoezi,mwili utahitaji kuchukua nguvu toka katika mafuta ili kujazia upungufu. Mfano unaweza ukatumia kj 10 kwa mazoezi ya dk 30 mpaka dk 60. Hivyo ukifanya mara kwa mara kama si kila siku utapungua tu uzito.
Mazoezi rahisi kufanya ni kukimbia kila jioni au asubuhi kwa umbali wa km 1 mpaka 2 zinatosha. Lakini unaweza kwenda katika kituo cha mazoezi jioni au ukanunua vifaa vya mazoezi na kufanya nyumbani kama unaweza.
  1. Mpango Sahihi wa Chakula-Chagua Kula Chakula Sahihi

kupunguza-uzito_chakula-1
Katika njia ya kwanza nimesema juu ya kiasi unachokula,hapa naelezea juu ya aina ya chakula unachotumia kinachangia uzito kuongezeka au vinginevyo.
Ulaji wa vyakula vingi vya wanga na mafuta ni chanzo kikubwa cha unene na uzito kuongezeka. Vyakula kama ugali,wali,mkate mweupe,bia na pombe za kienyeji zinazotokana na wanga (kimea) huchangia kuongezeka kwa uzito. Matumizi ya aina hii ya chakula ni muhimu kupunguzwa katika mlo wako.

Vitu vya kufanya katika mpango wa chakula:

  • Acha kula Vyakula vya Sukari

Sukari inayozidi mwilini toka katika vyakula hubadilishwa na kuwa mafuta. Vyakula kama chokuleti,biskuti,keki na vinyaji kama soda vina kiwango kikubwa cha sukari. Pia usitumie sukari nyingi katika chai na juisi.
  • Kula Mboga Mboga na Matunda Kwa Wingi

Mboga mboga ni nzuri kwa afya kwa ujumla lakini pia haina mafuta hivyo itakufanya kuingiza mafuta kidogo mwilini.
Matunda halikadharika hayapunguzi uzito moja kwa moja bali yatakufanya ushibe na usitamani kula kila mara kwani yanakata hamu ya chakula. Hivyo utaokoka na tabia ya kula kila mara ambayo huchangia sana kuongezeka uzito.
  • Acha Kula Kula Ovyo Nje ya Milo Maalumu

Uzito na kula kula hovyo ni marafiki wakubwa. Ukiona mtu ni mnene ujue anapenda kula. Ile kweli anakulakula ikimaanisha anakula kila mara na kila wakati chakula kinapokuwepo.
Anza leo kujenga tabia ya kula kidogo na katika milo muhimu mitatu.
  • Punguza Matumizi ya Chumvi

Ndiyo,chumvi inaongeza uzito. Sodiamu iliyomo katika chumvi inachangia katika mchakato wa kikemikali unaopelekea kuongezeka uzito. Tumia chumvi katika kiwango kidogo.
  • Tumia Chai ya Kijani

Umesikia kuhusu chai ya kijani (Green Tea), ni chai ambayo ni ya kijani na inasaidia kuondoa sumu za mwili (antioxadation). Hii inasaidia katika kusaidia mwili kuunguza mafuta katika njia inayoitwathermogenesis.
  • Tumia Chai ya Tangawizi

Tangawizi kama ilivyo chai ya kijani inafahamika kuongeza mmeng’enyo wa chakula tumboni hivyo kupunguza mrundikano wa mafuta yasiyotumika
  • Kunywa Maji Mengi

Maji yanachangia kuharakisha mfumo wa uvunjaji chakula tumboni na hivyo kupunguza mafuta yanayohifadhiwa.

Panga Malengo na Anza Kuchukua Hatua

Kupungua uzito kunahusisha suala la kubadili tabia. Kila mtu anajua ugumu wa kubadirisha tabia. Lakini kama unajali afya yako ni lazima ufanya maamuzi leo na weka malengo ya kuanza kufanya haya yaliyoelezwa hapa.
Mbuyu hauangushwi kwa siku moja,ila anza kupanda mimea mingine kuuzunguka na utaanza kudhoofika. Anzisha tabia mpya nzuri itakayokusaidia kupunguza uzito. Anza na hatua moja,inaweza ikawa kula kidogo au mazoezi kisha baadae ukafanya yote. Kuanza kuchukua hatua ni jambo gumu ila muhimu sana katika kutimiza lengo la kupunguza uzito.
Kama umeipenda mada hii basi mshirikishe na mwenzio na toa maoni yako au tufahamishe njia nyingine unazotumia kusaidia kupunguza uzito wa mwili. Asante kwa kusoma na nakutakia utekelezaji mwema.

No comments:

Post a Comment