Search This Blog

Saturday, 21 January 2017

UV-CCM Dodoma watuhumiana ubadhirifu

IMEANDIKWA NA SIFA LUBASI, DODOMA IMECHAPISHWA: 21 JANUARI 2017
http://www.habarileo.co.tz/images/resized/images/
KAMATI ya utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Taifa imeombwa kuwasimamisha uongozi watendaji wa Umoja wa Vijana wa CCM mkoa wa Dodoma akiwemo mwenyekiti wake wa mkoa kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umoja huo na matumizi mabaya ya fedha.
Pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa, Henry Msunga wengine ni Katibu UVCCM, Salum Kidima na Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Egla Mwamoto. Wametaka kusimamishwa huko kuambatane na uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili viongozi hao katika fedha na matumizi ya mamlaka.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ikiwa ni siku moja mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kikanuni cha baraza la vijana mkoa wa Dodoma , Mwenyekiti wa UVCCM Chamwino, Fransis Gombo, alisema wamefikia uamuzi wa kutoa ombi hilo kupitia vyombo vya habari baada ya kuona hoja zao hazifanyiwi kazi huku jumuiya hiyo mkoani ikizidi kudidimia.
Akiwa na wajumbe wengine katika mkutano huo Gombo alisema tangu mwaka 2014 viongozi hao hawajaitisha kikao chochote cha kikanuni. Gombo alisema kumekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za jumuiya ikiwamo sehemu ya maandalizi ya harusi ya mwenyekiti.
Aidha alisema kuna mradi wa vibanda zaidi ya 100 vilivyopo katika ndani ya eneo la soko la Sabasaba ambavyo vinamilikiwa na UVCCM mkoa wa Dodoma, lakini umeonekana kama hauna mwenyewehuku anayekusanya fedha akiwa hajulikani.
Imedaiwa kwa waandishi wa habari na Gombo kwamba wapangaji wa vibanda hivyo hulipa kiasi cha laki moja na nusu mpaka laki mbili, lakini viongozi wao wamekuwa wakiwapa taarifa wajumbe kuwa wapangaji wanalipa kodi kati ya Sh. elfu kumi mpaka elfu ishirini.
Aidha msemaji huyo amesema kwamba kuna haja kwa uongozi wa Chama kumuondoa Kaimu Katibu wa CCM Mkoa, Jamila Yusufu, kwa madai kuwa hawana imani naye na amepoteza sifa ya kuwa mlezi wa jumuiya hiyo.
Pia wamemtuhumu katibu huyo, kwa kuvuruga kikao cha baraza kilichofanyika juzi, Januari 19 mwaka huu kwa kuegamia upande mmoja na kumuondoa mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Dodoma ndani ya kikao kabla kikao hicho hakijamalizika.
Akizungumzia tuhuma hizo Mwenyekiti wa UVCCM mkoa Msunga, alikanusha kuhusika na tuhuma zozote huku akisema kuna utaratibu wa kushughulika na tuhuma za ubadhirifu ndani ya chama unaohofiwa ama unaofanywa na viongozi.
Mwenyekiti huyo, alisema, kuhusiana na tuhuma za fedha za jumuiya kutumika katika harusi yake hana taarifa na jambo hilo, labda kama atapewa taarifa kuwa kuna fedha zilitolewa na kutumika, lakini binafsi hajui chochote anachofahamu ni kwamba harusi yake aliigharamia mwenyewe na ilikuwa ya gharama kubwa.
Kuhusu vibanda vya sabasaba alisema, kodi inayotozwa ni Sh10,000 kwa kibanda kimoja ambapo baadaye iliongezwa kufikia Sh20,000 ambayo ndiyo inayotozwa mpaka sasa.
Pia alisema kikao cha baraza cha Januari 19 mwaka huu kiliahirishwa mpaka Januari 26, mwaka huu, kutokana na baadhi ya mambo kutokamilika.
Naye Kaimu Katibu wa CCM mkoa, Jamila, alipohojiwa kuhusiana sakata hilo, alisema, Chama kina utaratibu wake mambo ya chama sio ya kuzungumza kwenye vyombo vya habari, huku akidai kuwa fukuto hilo la umoja wa vijana mkoa wa Dodoma, huku akigoma kuendelea kutoa ufafanuzi zaidi kwa madai kuwa yuko katika maandalizi ya uchaguzi wa Udiwani Kata ya Ng’ambi.


Mjumbe wa Baraza kuu la UVCCM Taifa, Egla, alipohojiwa kuhusiana na maazimio hayo, alitaka kujua ni kikao kipi kilichoazimia maazimio hayo kwa kuwa yeye anachofahamu ni kwamba kikao kilichokaa Januari 19 kiliahirishwa na kitafanyika tena Januari 26 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment