Search This Blog

Saturday, 14 January 2017

‘Msikubali kumpa kadi za kupigia kura’

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi

By Aurea Simtowe, Mwananchi mwanachipapers@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Ramadhan Kailima amewataka wananchi wasikubali kumpa kadi ya kupigia kura mtu yeyote isipokuwa kuionyesha kwenye kituo cha kupigia kura siku ya uchaguzi.
Sambamba na hilo, Kailima amewaambia waandishi wa habari kuwa ACT-Wazalendo na vyama vingine vya siasa vyenye wagombea katika uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge, kutumia haki zao kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa kamati husika.
“Kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya maadili ya uchaguzi, Tume inavikumbusha vyama vya siasa kuwasilisha malalamiko yao katika kamati ya maadili ngazi ya kata ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa ukiukwaji wa maadili,”amesema Kailima.
Amesema kama chama hakitaridhika na uamuzi utakaotolewa na kamati ya maadili ngazi ya kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7(a) ya maadili ya uchaguzi awasilishe rufaa kwa msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo ndani ya saa 24 tangu uamuzi wa ngazi ya kamati ya kata kutolewa.
Kailima amesema endapo chama bado hakijaridhika na uamuzi ya ngazi ya jimbo, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7(b) na (c), kina fursa ya kuwasilisha rufaa kamati ya maadili ya ngazi ya taifa au ngazi ya rufaa ambayo ni NEC.
“Kwa mujibu sehemu ya 5.7(e) ya maadili ya uchaguzi, kama chama au mgombea hakuridhika na uamuzi ya kamati ya rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malalamiko yake mahakamani baada ya uchaguzi kufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” alisema.

No comments:

Post a Comment