Dini ya kweli ni ipi?
Ninayo miaka mingi katika medani hii ya uandishi nikijikita zaidi katika kona ya uchambuzi wa masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Katika uandishi wangu huo nimekumbana na maswali ya kila aina kutoka kwa watu wa kila aina toka pande mbalimbali za sayari hii dunia.
Baadhi ya maswali nimeyajibu na mengine kwa namna moja au nyingine nilishindwa kuyajibu. Hii ni kutokana na mchepuo, mtazamo au shabaha ya muuliza swali. Lakini pia huwa ninaangalia mantiki ya swali kama inagusa jamii iliyo pana au la!
Leo moyo wangu umenisukuma kujibu swali hili la dini ya kweli ni ipi labda kiu ya waulizaji inaweza kupoa.Wameniuliza swali hili kupitia simu yangu ya mkononi. Wameandika hivi, “Bwana Bollen Ngetti, wewe ni mchambuzi mahiri na makini wa masuala ya kijamii na tunaamini dini ni sehemu ya jamii, hivi dini ya kweli kati ya Uislamu na Ukristo ni ipi?
Ukiangalia kwa macho ya firka utabaini kuwa swali hili lina mambo laki nyingi ndani yake na yumkini tusiyamalize leo wala siku za usoni. Hii ni kutokana na wauliza swali kunilazimisha nichague dini moja ya kweli kati ya mbili walizoainisha yani Uislamu na Ukristo.
Bila shaka wauliza swali watakuwa vijiweni, darasani, kwenye mihadhara, kwenye daladala, ndani ya sinagogi au hata kwenye halfa ya vileo na hakuna shaka wako kwenye mabishano makali juu ya dini ya kweli ni ipi?
Na ili mabishano yao yafikie tamati salama ndio maana wameamua kunitupia swali hili labda upande mmoja unaweza kuondoka kidedea!
Niwashukuru wauliza swali kwa kunipa heshima hiyo kwani swali hili wangeulizwa mapadre, wachungaji, masheikh na wanazuoni waliobobea katika masuala ya teolojia na dini, lakini wakaamua kuniuliza mjoli niliye mithili ya kichuguu mbele ya mlima Kilimanjaro katika muktadha wa elimu ya dini.
Hata hivyo katika maandiko yangu siku za nyuma niliwahi kusema kuwa sisi kama binadamu walio huru tunapaswa kutumia nishati ya bongo zetu kufikiri, kutafakari na kuamua kama moja ya sifa inayotutofautisha na wanyama wengine.
Hebu na tutumie uwezo huo huo kufikiri, kutafakari na kuamua juu ya dini ya kweli.
Hata hivyo kutokana na mgomo baridi wa fikra waliouonyesha wauliza swali, nimejikuta wakinibana mbavu ili nitoe jibu kwa kuchagua aidha kushoto ama kulia.
Lakini pia swali hili linaweza kuwa na mtego ndani yake ili niseme dini zote mbili ni za kweli ama za uongo! Binafsi swali hili limenifumbua macho kuwa kumbe wapo watu wanaoamini kuwa kuna dini moja ya kweli na zingine ni za uongo!
Kwa kuwa dini hizi huongozwa na imani ya uwepo wa Mungu, hivyo kama kuna dini ya kweli basi kuna Mungu wa kweli na Mungu wa uongo kwa dini ya uongo. Kwa mantiki hiyo tunaye Mungu wa kweli na Mungu wa uongo.
Hapa ndipo tofauti yetu na kondoo unapo paswa kudhiirika bayana tukitafakari kwa kina na mapana matilaba haya ya dini. Kinyume cha hapo ni kupoteza nguvu nyingi katika mabishano ambayo hata ujinga wa mtu uliokuwa umejificha katika nafsi sasa unaweza kujidhiri nje naye akachekwa.
Na mimi niwaulize wauliza swali kwa nini wamenipa chaguo la dini hizi mbili tu? Mbona dunia imesheheni dini na taratibu za kiimani na kiroho nyingi mno?
Kwa nini wanataka nitoe msimamo wangu kwa dini mbili tu ya Uislamu na Ukristo kama si kunipofusha fikra nisione mbali?
Tulichukulia mfano wa bara letu la Afrika pekee kila kabila ina taratibu zake murua za kiimani na kiroho, kwani nini hawa wasomaji wangu wasiniulize juu ya imani hizi zipi za kweli? Mungu wa kweli ni wa kabila gani?
Hata hivyo, swali hili linatuzalishia swali jingine : hivi, hapa duniani kuna dini ya kweli hasa? Na, je, kuna dini ya uongo? Na ni nani mwenye mamlaka ya kuamua dini moja kuwa ya kweli na zingine kuwa za uongo? Anatumia vipimo gani vilivyothibitishwa na nani?
Labda nina ufinyu wa fikra au ujinga wangu umefunika. Lakini mjinga kugundua na kukubali ujinga wake si ni hatua ya mwanzo ya kuacha ujinga na kuerevuka?
Nasema hivi kwa sababu sielewi, hivi, mtu anaposema Ukristo au Uislamu huwa anamaanisha nini? Je, kama Wapentekoste ni Wakristo, Wakatoliki nao ni Wakristo?
Mfano ; Wakatoliki wanaamini ubatizo wa mtoto mdogo na Kristo ndiye anawaongoza kufanya hivyo wakati Wapentekoste wanaamini ubatizo ni kwa mtu wazima tu tena kwa kuzamishwa ndani ya maji mengi kama alivyobatizwa Yesu (mwasisi wa Ukristo) katika mto Jordan.
Sasa inawezekana ukatoliki ni upentekoste vikawa ni Ukristo kweli?
Je, wale Wa-Adventista Wasabato wanaoamini kuwa siku takatifu ya ibada ni Jumamosi tu ni Wakristo sawa na Walutheri wanaoabudu siku ya Jumapili?
Je, Mashahidi wa Yehova wasioamini utatu mtakatifu kuwa ni Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu ni sawa na wanaoamini utatu mtakatifu kama mafundisho ya kweli ya Biblia?
Kama wote ni Wakristo, kwa nini wengine waamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na wengine wadai Yesu ni Mungu? Kwa nini wengine waamini Yesu alitumwa duniani kuwaokoa wanadamu na wengine waamini alijituma binafsi kumwokoa mwanadamu aliyepotea?
Inawezekana vipi mitizamo hii miwili inayokinzana yote kuwa ya Kikristo ilhali wote wakitumia msaafu wa Biblia?
Yapo madhehebu yanayoruhusu wanawake kuwa wachungaji, wainjilisti, wahubiri: yapo mengine yanayokataza, yapo madhehebu yanayoruhusu ndoa za jinsia moja lakini wote wanapunga mapepo kwa jina la Yesu Kristo, Je, huyo Kristo hana falsafa moja inayoongoza dini yake?
Kama ndio hivyo,neno “Ukristo” linaweza kuwa na maana moja huku wafuasi wake wakitofautiana kiteolojia, kifalsafa, matendo, tambiko na tafsiri ya maandiko?
Leo kila kona ya nchi yetu hasa maeneo yenye mwamko wa kiuchumi kumeoteshwa madhehebu lukuki kila moja ikiwa na staili yake ya kuwahadaa wafuasi wake kwa jina la Yesu Kristo (hii nitaijadili huko mbeleni)
Lakini bado niwaulize wasomaji wangu waliniuliza Ukristo upi hasa?
Tukirudi kwa Uislamu nao kama Ukristo, ndani yake kuna makundi si haba. Tafsiri ya mafunzo na maisha ya mtume sio sare.
Vijana waliolipua mabomu nchini Uingereza mwaka 2005 – walitamba na kusema wao ni waislamu na kazi waliyoifanya iliwapa thawabu mbele za Allah!
Wakati huo huo wapo Waislamu waliodai hao vijana pamoja na wafuasi wa Osama bin Laden wa mtandao wa Al-queda wameuteka nyara Uislamu na kuuchafua. Sasa unajiuliza Je, “Uislamu” ni mjumuiko wa wanaojitoa mhanga kuua watu wasio na hatia na wasiojitoa mhanga?
Ndani ya Uislamu wapo waumini wa Shia na Suni ambao wote wanatofautiana katika taratibu za ibada na itikadi.Wapo pia kundi la Ansali Sunna wanaoamini uvaaji wa nguo ndefu ni kupoteza udhu (usafi) wakati wale wa Imamu Shaffir wakishahadia nguo ndefu kama njia ya kujisitiri mwili na kumpendeza Mungu.
Wapo waislamu wanaofunga sala kwa kuweka mikono kifuani huku wengine wakiweka tumboni. Lakini wote wanajiita Waislamu!
Ndani ya Shia kuna wale wanaoamini kuwa kuna maimamu 12 na wote hawajawahi kutenda dhambi. Kuna jingine linaloamini kuwa maimamu halisi walikuwa saba tu (Waismailia).
Dhehebu la Zayid nao wanaamini maimamu walikuwa ni watano tu na si kweli hawakuwahi kutenda dhambi.
Ukienda Marekani utakutana na waislamu weusi wanaamini wao ndio waislamu halisi na si Shia au Sunni. Hawa ni wale wanaojiita Taifa la Waislamu (Nation of Islam) linaloongozwa na mhubiri Louis Farrakhan.
Mgawanyiko huu ni mkubwa sana. Sasa tunajiuliza tunaposema Uislamu tunamaanisha kundi lipi?
Lakini wauliza swali wanashindwa kujua kuwa sisi tumekuwa wafuasi wa dini hizi pepe kutokana na mambo mengi ya kihistoria na kijiografia na uhalisia.
Mfano; ni vigumu kumkuta Mjaluo wa Musoma kuwa Muislam ilivyo vigumu kumkuta Mpemba si Muislamu kwani Waarabu walitia nanga visiwani Pemba.
Ufahamu wetu mdogo katika masuala ya roho ni sawa na falsafa ya Astria ya shimo iliyoelezwa Wayunani wa kale.
Ulielezwa hivi; wapo watu ambao maisha yao yote waliishi shimoni kwenye giza. Na kila watu walipopita nje vivuli vyao vilionekana ndani nao wakaamini vivuli vile ndio watu halisi hadi mmoja wao alipotoka nje na kuuona mwanga wa jua.
Lakini aliporudi shimoni kutokana na mwanga wa jua uliompiga usoni hakuweza kuona vizuri. Ndipo wenzie walipomwambia “sasa unaona huko nje sio kuzuri kwani huwezi kuona tena”.
Huyu Bwana akaamua kutoka mle shimoni na kuishi nje kwenye mwanga wa jua na kuacha wenzie wakiendelea na maisha ya shimoni ya kuamini vivuli kuwa watu.
Ninajaribu kuwafananisha wauliza swali na watu waishio shimoni wanaodhani dini wanazoamini na kuabudu ndio za kweli na wasioamini dini zao ni wapotevu.
Huu ni upofu na ujinga ambao hata ukitwangwa kwenye kinu hauwezi kumtoka mtu!
Niliwahi kuandika kuwa ujio wa dini hizi za mashariki ya kati yani Uislamu na Ukristo ulitokana na mchakato mzima wa ukoloni mkongwe ambao hatunabudi kupingana nao kwa nguvu zote.
Upo usemi wa kale usemao;’’Mwafrika anaenda kanisani au msikitini na msaafu kwapani lakini hawezi kusahau hirizi kiunoni.’’ Huu ni uthibitisho kuwa dini pepe hazijafua dafu mbele ya dini au imani za Kiafrika zilizoitwa ushenzi na washenzi hasa.
Tuna shuhudia viongozi wetu wa kisiasa wakikesha katika nyumba za ibada lakini kamwe hawawezi kuacha kwenda kwa sangoma kutizama upepo wa uchunguzi ujao.
Hivyo basi kuniuliza dini ya kweli kati ya Uislamu na Ukristo ni kutonitendea haki za msingi kifikra.
Sote tunapapasa kama kipofu aliegusa sikio la tembo na alipoulizwa unamjua tembo? Akasema; “ndio, tembo anafanana na beseni kubwa la kuogeshea watoto”.
Karl Max, muumini wa sosholojia alibainisha,’’dini ni ulevi, umlevya mtu kama bangi.’’ Nimelishuhudia hili pale Manzese darajani jijini Dar-es-salaam ambapo watu wana shindana kutetea dini ngeni barani Afrika kiasi cha kutokwa mapovu mdomoni mithili ya mgonjwa wa kifafa!
Dini ngeni imetumika sehemu nyingi duniani kudhoofisha jamii mbalimbali kisiasa, kiuchumi na kimahusiano.
Mwandishi Chinua Achebe anasema; “mtu mweupe ni mjanja sana, tazama aliingia kwetu, nasi tukampokea; amedhoofisha watu, hatuwezi tena kutenda kwa umoja wetu kwani hata imani zetu zimedhoofishwa”.
Haya niyasemayo yametokea nchini Ghana hivi karibuni baada ya Ghana kuwa pagumu kuingilika kwa lengo la kupora rasilimali hasa madini.
Marekani na maswahiba wao wakaamua kuanzisha madhehebu ya kilokole kila kona huku injili kuu ikiwa ni; “msihangaikie mali ya dini kwani thawabu yenu iko mbinguni ambako Yesu alienda kuandaa makao”.
Leo asilimia 90 ya vyombo vya habari nchini Ghana vinamilikiwa na madhehebu ya kiroho yenye asili ya Marekani.
Hapa ndipo kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini ya Barik inayomilikiwa kwa asilimia kubwa ya hisa na familia ya Rais George Walker Bush ilipoanza kuchota dhahabu hadi sasa wamehakikisha nchi ya Ghana imebaki mahandaki (sasa mapango).
Sasa Barki imehamia Tanzania sambamba na ujio wa kila aina ya kanisa inayoponya “mapepo” kwa jina la Kristo.
Hapa ndipo tunapojiuliza Ukristo wa kweli ni upi? Huu wa sasa au ule wa kihafidhina?
Ni ushahidi upi wa kitafiti unaoonyesha imani zetu za kiafrika ni ushenzi kiasi cha wauliza swali wasizihusishe kujua dini ya kweli kama huku si kutekwa nyara na minyororo ya ukoloni mkongwe?
Wauliza swali wanapaswa kuketi kitako na kutafakari upya swali lao kwani huko nyuma niliweza kubainisha uhusiano baina ya ubongo, imani na akili katika maamuzi ya fikra yanayoongoza matendo ya nje.
Dini yangu siyo ya kweli, dini yako nayo si ya kweli, hata yule naye dini yake siyo ya kweli hivyo basi, hili la dini ya kweli ni ipi ni juu yako mwenyewe na nafsi yako. Naomba kutoa hoja!
Bollen Ngetti ni mchambuzi wa masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment