Na Mwandishi wetu, Desemba 7-13
MTOTO Mary Richard Salugole (6), ambaye alikuwa na maradhi ya kupooza kwa zaidi ya mwaka mmoja, amesema umefika wakati ambao wasioamini kuwa Yesu Kristo anaponya, waache ubishi ili wamwendee Yesu kama suluhisho pekee la matatizo yote yakiwemo maradhi.
Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi yaliyofanyika wiki iliyopita huko Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, mtoto huyo aliwataka wasioamini uponyaji wa kiungu, wapate somo kutokana na uponywaji wake yeye.
Alisema: "Hakuna kitu chochote ambacho kina uwezo wa kushindana na mapenzi ya Mungu na hasa kama mtu ana imani thabiti bila kutetereka na kuacha kumsikiliza Ibilisi anayewatafuta na kuwakatisha tamaa watu wa Mungu."
Kufuatia kuponywa kwa mtoto huyo, baba yake aliamua aandae tafrija ya kumshukuru Mungu na kushuhudia matendo yake makuu kwa familia yao hususan kwa mtoto huyo pekee kwenye familia hiyo, ambayo ilifanyika huko Kibamba nyumbani kwao.
Akiielezea historia ya matatizo ya mtoto huyo, baba yake alisema kwamba ilikuwa siku moja usiku wa saa saba, mtoto huyo aliomba kupelekwa kujisaidia lakini muda mfupi baadaye ghafla alijisikia akiishiwa nguvu maungoni na kushindwa hata kushika kitu au kusimama.
Aliendelea kusema kuwa usiku huo walianza maombi na kulipokucha walimpeleka Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani kwa matibabu.
Mzazi huyo akasema kutokana na imani thabiti ya mtoto huyo kwa Mungu, aliwapa nguvu wazazi wake na hasa alipokuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba atapona tu kwa jina la Yesu, kwa hiyo wasiwe na wasiwasi wowote juu ya ugonjwa huo.
Mzazi huyo akasema kwamba hata hivyo baada ya miezi michache, ndipo walipoanza kuona uwepo wa Mungu ukiwashukia huku wakimwona mtoto wao huyo akianza kusogeza mkono ambapo baada ya siku tatu alisogeza mkono wa pili na hatimaye alirudi katika hali yake ya kawaida kabisa. "Mwanangu alikuwa akitusihi tuwe na imani thabiti na kuamini ya kuwa yeye ameshapona kwani alisema kuwa kinywa kikiripo basi tendo hilo hutendeka kama vile kinywa kilivyokiri," alisema baba wa mtoto.
Awali katika tafrija hiyo, baba wa mtoto alisema kwamba aliandaa sadaka maalum katika azma yake ya kuondoa (kutimiza) nadhiri yake kwamba kama mtoto wake atapona maradhi yaliyomsibu, angemtolea Bwana sadaka ya shukurani.
Kwa upande wake mtoto huyo alisema kwa msisitizo: "mimi ninaamini kuwa Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu na kutukomboa kutoka katika shimo la mauti kwa hiyo nina imani ya kuwa shetani asingeweza kunishinda kwa kuwa ninaye Yesu aliyenifia kwa ajili ya ukombozi wangu, shetani ameshindwa."
No comments:
Post a Comment