Search This Blog

Saturday, 14 January 2017

Mchawi atangaza vita na mchungaji


Na Mwandishi Wetu, Dodoma. Oktoba 19 - 25 
VITISHO dhidi ya watenda kazi wa Injili ya Yesu, vinavyofanyika duniani kote, vimeendelea kujitokeza na sasa wala si mbali tena ni hapa hapa nchini kwetu ambapo mchungaji mmoja wa kipentekoste ametishiwa kuuawa eti kwa kuwa anakwamisha biashara ya uchawi kwa kuwahubiria watu Injili hata wakaamua wasikanyage tena kwenye ushirikina.

Mtumishi wa Mungu aliyetishiwa kutolewa roho, ni Mchungaji Amos Mchagalo wa TAG, kijijini Zamahelo, mjini hapa, akidaiwa kwamba anahubiri mno na sasa wateja wanakosekana kutokana na kuhubiri kwake.

Mchungaji huyo ameliambia gazeti hili kwamba mchawi huyo maarufu kijijini hapo (jina linahifadhiwa), ameonya kwamba kwa kuwa sasa watu wengi wanaokoka na kuachana naye, biashara yake itayeyushwa na Injili hali itakayomnyima riziki yake kwa njia hiyo haramu ya kupata riziki.

Mchungaji Mchagalo akasema kwamba kigagula huyo mwenye takriban miaka 70, akishirikiana na mjukuu wake, wamekuwa maarufu kijijini hapo huku wakiendelea kupeleka mkono kinywani kwa kazi yao chafu machoni pa Mungu.

Mchungaji huyo akasema kwamba kutokana na maombi kwa jina la Yesu, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Bibi Marysiana Maweza, ambaye alikuwa na mimba iliyodumu kwa miaka miwili na nusu bila ya kujifungua ingawa alihangaika kwa washirikina wengi kama mchawi huyo, alijifungua mtoto aliyepewa jina la Syliana ambaye ni mzima wa afya. Akasema kwamba inaaminika mimba hiyo ilipigwa juju na wachawi ili mhusika asijifungue kwa wakati upasao.

Baada ya tukio hilo lililomwondolea mzigo na kero za ujauzito, Mama Syliana akaamua aokoke na sasa amejiunga nan kanisa la TAG kijijini hapo. Mchungaji huyo ametoa wito kwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo kushirikiana ili kuvunja ngome ya wachawi kijijini hapo.

No comments:

Post a Comment