Uzito uliozidi ama uzito uliokithiri unahusishwa na magonjwa mbalimbali kama shinikizo la damu, kisukari n.k. Hivyo wataalam wa afya wamekuwa wakishauri mara kwa mara watu kupunguza uzito. Lakini wakati mwingine mtu anaweza akajiuliza atajuaje kama uzito wake ni hatari? Kama ungependa kujua uzito wako ni sawa ama siyo sawa tembelea kituo chochote cha afya. Utapimwa urefu na uzito wako kisha utaambiwa kama uzito wako ni mkubwa ama la. Hapo sasa utajua kama unahitaji kuongeza uzito ama kupunguza uzito.
Mambo ya kuzingatia kama unataka kupunguza uzito
1. Fanya maamuzi ya dhati- kwanza kubali unahitaji kupungua vilevile tambua kwamba kuna vitu ambavyo vitabadilika katika maisha yako. kwa mfano vyakula.Hivyo jiandae kabisa kuepuka vitu kama pombe, soda, sigara, nyama nyekundu, vyakula vilivyokobolewa n.k
2. Badili mfumo wa maisha- Jiandae kubadili mfumo mzima wa maisha yako. Kuwa mwangalifu na vyakula unavyokula, kama ulikuwa hufanyi mazoezi basi ni wakati wa kuanza kufanya mazoezi.
3. Tafuta njia salama ya kupunguza uzito. Hakikisha haujinyimi chakula kabisa bali punguza taratibu kiwango ulichokuwa unakula. Hakikisha unakula mlo kamili.
4. Sasa upo tayari. Anza taratibu kuelekea kupunguza uzito. Kila la kheri!
Punguza uzito kwa kutumia maji
Jinsi ya kutumia maji kupunguza uzito:
1. Pindi tu unapoamka asubuhi- kunywa kati ya glasi mbili hadi tatu za maji (kati ya 300ml na 600ml)
2. Baada ya saa moja (Kabla ya kifungua kinywa)-kunywa kati ya glasi moja mpaka mbili za maji (kati ya 250ml na 500ml)
3. Kila unapokunywa kikombe cha chai/kahawa-kunywa glasi moja ya maji (kati ya 100ml na 250ml)
4. Dakika ishirini (20) kabla ya kila mlo- Kunywa kati ya glasi moja mpaka mbili za maji (kati ya 250ml na 500ml)
5. Masaa mawili (2) kabla ya kwenda kulala -Kunywa kati ya glasi mbili mpaka tatu (kati ya 300ml na 600ml)
Zaidi ya maji kukusaidia kupunguza uzito lakini vilevile yatakuwezesha kuwa na ngozi nzuri na nyororo. Jitahidi kubadili mfumo wa maisha yako na kufanya maji kuwa sehemu ya maisha yako na si tu kwa ajilli ya kupunguza uzito.
Chanzo: www.stevenaitchison.co.uk
Mazoezi ni Muhimu
Mazoezi kwa ujumla ni muhimu sana kwa kila mtu na si kwa wale tu wanaotaka kupunguza uzito. Ila kwa wale wenye nia ya kupunguza uzito ni muhimu zaidi. Kumbuka hata kama wewe ni mwembamba bado unahitaji kufanya mazoezi kwa ajili ya afya yako. Watu wanaohitajika sana kufanya mazoezi ni wale ambao hawafanyi kazi za kuushughulisha mwili, kazi ambazo si za kutumia nguvu. Kwa mfano: wale wanaotumia magari kwenda sehemu zao za kazi na wakishafika hukaa tu kwenye madawati yao ya kazi siku nzima na mwishowe jioni hurudi tena nyumbani wakitumia magari. Kama upo kwenye mfumo huo wa maisha bila shaka unahitaji kufanya mazoezi angalau hata kwa nusu saa kila siku na hakikisha unatoka jasho. Unaweza kufanya mazoezi yafuatayo:
1. kutembea- Unaweza kutembea kwa mwendo wa haraka ama taratibu kadiri ya mwili unavyokuruhusu ama ukaanza taratibu na kila siku ukawa unaongeza spidi.
2. kukimbia- Mazoezi ya kukimbia pia ni mazuri sana kwa mwili wako. Unaweza ukaamka asubuhi na kukimbia kwa dakika thelathini (30) kabla ya kwenda eneo lako la kazi ama pengineko. Anza taratibu kisha ongeza spidi kadiri mwili utakavyokuruhusu.
3. Kuruka kamba- kuruka kamba pia ni mazoezi mazuri sana. Tafuta kamba yako. Anza kwa kuruka labda mara ishirini ama thelathini kisha jitahidi kila siku kuongeza idadi kadiri mwili wako unavyokuruhusu.
4. Michezo- Pia unaweza kushiriki katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, tennis, kuogelea n.k hii pia ni njia nzuri ya kuuchangamsha mwili.
5. Gym (Vituo vya kufanya mazoezi)- hii ni sehemu maalumu kwa ajili ya kufanya mazoezi ambapo huwa na mwalimu wa mazoezi ambaye atakuonyesha na kukushauri aina ya mazoezi ambayo yatakufaa. Kufanya mazoezi katika sehemu hii ni nzuri sana kwasababu hukukutanisha na watu wengine na hivyo hukupa hamasa zaidi ya kufanya mazoezi kuliko ukifanya mazoezi peke yako.
6.Jiunge na vikundi vya kukimbia (jogging clubs)- Unaweza pia ukajiunga na vikundi vya kukimbia, mara nyingi ukifanya mazoezi na wenzako huwa rahisi zaidi kuliko kufanya mwenyewe inatia uvivu.
7. Kuendesha baiskeli- baiskeli pia ni moja ya zoezi zuri hususani kwa wale wenye lengo la kupunguza mwili. Hii haimaanishi yule asiyetaka kupunguza uzito haruhusiwi la hasha kila mtu anaweza kufanya zoezi hili na akaweka mwili wake sawa (fit).
Hayo tu ni baadhi ya mazoezi unayoweza kufanya ukiwa unataka kupungua uzito ama ukitaka tu kutunza afya yako. Kama nilivyosema awali mazoezi ni muhimu sana kwa kila mtu. Ni muhimu sana ufanye mazoezi kwa muda wa dakika thelathini (30) ama zaidi na hakikisha pia unatoka jasho. Ni muhimu mno kutoka jasho. Hakikisha pia unakunywa maji ya kutosha ukiwa unafanya mazoezi.
Chanzo:Dr. Ally Mzige (Imtu)
No comments:
Post a Comment