Mbuyu ni jina la Kiswahili la mti wenye asili ya kale wa jamii ya Adansonia, na kuna aina tisa katika
jamii ya mibuyu ambapo aina sita zina asili ya kisiwa cha Madagascar na aina mbili ina asili ya barani Afrika na Ghuba ya Uajemi na moja ina asili ya bara la Australia. Mti wa mbuyu una uwezo mkubwa wa kuhifadhi maji, na huifadhi takriban kiasi cha lita 100,000 na kuufanya mti huu kuweza kukabiliana na hali ya ukame hususan katika maeneo yaliyo na hali ya ujangwa. Uwezo wa kuhifadhi maji mengi hutokana na mtii huu kupukutisha majani yake nyakati za kiangazi.
Unga wa ubuyu uliokaushwa wa mti wa jamii ya A digitata huwa na virutubisho vingi kama wanga, protini, Vitamini B2(Riboflavin),Kalshamu,Magnesiamu,Potasiamu, Chuma, Protini muhimu, Vitamini C na aina nyinginezo za virutubisho.
Moja ya umuhimu mkubwa kiafya wa tunda la ubuyu ni uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili, kuimarisha mifupa, kusaidia mfumo wa umeng’enyaji tumboni, kupunguza maumivu na uvimbe na kusisimua utengenezaji wa seli na tishu mpya . Pia kusaidia kupunguza shinikizo la damu na kuzuia magonjwa sugu.
Sababu inayolifanya tunda la mbuyu kuwa la pekee ni kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha virutubisho kama madini, vitamini na protini. Ubuyu una kiwango kikubwa pia cha madini ya chuma, ambayo ni sehemu muhimu ya protini ya haemoglobin inayohusika na usafirishaji wa hewa ya Oxyjeni na protini hii ni sehemu ya seli hai nyekundu ya damu. Ulaji wa ubuyu waweza kutuepusha na ugonjwa wa kupungukiwa damu ujulikanao kitaalam kama Anemia. Matumizi yake ni pamoja na kuupatia mwili nishati inayoitajika ili mgonjwa apone haraka.
Kiwango kikubwa cha madini ya Potasiamu katika tunda la ubuyu, kunapelekea tunda hili kuwa na manufaa kwa afya ya moyo. Madini ya Potasiamu husaidia kutanua mishipa ya damu na ateri, na matokeo yake huusadia kuupunguzia moyo kutumia nguvu nyingi katika kusukuma damu . Kutanuka kwa mishipa ya damu kutapunguza shinikizo la damu kwa hiyo kutatuepusha na magonjwa ya moyo yakiwemo yale ya kukakamaa kwa mishipa ya damu, shambulizi la moyo na magonjwa mengine ya moyo yaliyo hatari.
Uimarishwaji wa mifupa kutokana na ubuyu ni dhahiri kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya Kalshamu na Magnesiamu. Kama una wasiwasi wa udhoofu wa mifupa kutokana na umri mkubwa, waweza kuongeza ubuyu katika orodha ya lishe yako kwani itakusaidia kuimarisha mifupa unapoelekea uzeeni. Kwa watoto madini haya ni muhimu kwa kuwa huimarisha mifupa na meno, na yatawaepusha na ugonjwa wa kupinda mifupa ujulikanao kama Rickets.
Ubuyu una aina mbili za fiba (nyuzi lishe), zile zinazochanganyika na maji na zisizo changanyika na maji, na hii ndio sababu ubuyu umekuwa ukitumika kwa miongo mingi kusaidia kurekebisha mmeng’enyo wa chakula tumboni na kuondoa maumivu yasababishwayo na matatizo ya mmeng’enyo. Fiba hizi husaidia pia kurekebisha kiwango cha sukari katika damu, kiwango cha lehemu na kuboresha afya ya moyo. Fiba pia husaidia kurekebisha kiwango cha bacteria wenye faida tumboni na kuboresha mmeng’enyo.
Viondoa sumu(Anti-oxidant) vimesheheni katika ubuyu, na hii inamaanisha kuwa tunda hili husaidia kutukinga na aina nyingi za magonjwa pamoja na saratani.
Vitamini C ni aina ambayo hupatikana kwa wingi katika ubuyu, na uimarishwaji wa kinga ya mwili hutokana na kuwepo kwa vitamini C(Ascorbic acid)kwa wingi. Kwa hiyo ubuyu husaidia kuongezeka kwa seli hai nyeupe za damu na kusisimua kinga ya mwili kupambana na vijimelea vya magonjwa.
Vitamini C pia husaidia katika utengenezaji wa Kollajeni(Collagen), protini ambayo husaidia kukarabati seli, tishu, mishipa ya damu na mifupa. Kiwango kikubwa cha Vitamini C sio tu kwamba huimarisha kinga ya mwili, bali huusaidia mwili kuwa na utendaji kazi bora wa mifumo mbalimbali i na hupelekea kupona haraka kwa magonjwa, majeraha hata kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji.
Nchini Tanzania kabila la wasandawe hutumia unga wa ubuyu katika uchachushaji wa juisi ya miwa kutengeneza bia na majani yake hutumiwa kama mboga.Unga wake hutumika na watu wengi kutengeneza juisi yenye ladha ya kuvutia. Pia ubuyu huliwa kwa kumung’unya mbegu zake hususan na watoto na kina mama.
Nchini Zimbabwe unga wa ubuyu hutumika kutengeneza chakula cha asili pamoja na kuchanganya kwenye uji ili kuongeza ladha.Nchini Malawi wakina mama wameanzisha ujasiriamali wa uvunaji wa ubuyu kwa ajili ya biashara na hujipatia kipato kinachowasaidia kulipa ada za shule za watoto.
Tahadhari
Mafuta ya mbegu za tunda la mbuyu yaweza kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali ijulikanayo kama Cyclopropenoid fatty acids (CPFA), ambayo katika tafiti nyingi imeonekana kusababisha ugonjwa wa ini na hata saratani. Pia ni vyema kuhakikisha unga wa ubuyu unaandaliwa katika mazingira au hali ya usafi ili kuepuka maambukizi ya magonjwa.
No comments:
Post a Comment