Search This Blog

Thursday, 12 January 2017

TANZANIA: Nyongeza ya Mishahara 100% kwa Faida ya Nani?

Na Marko Gideon 

Hivi karibuni serikali ilitangaza kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi kwa asilimia 100%. Hatua hii imekuja baada ya msuguano wa muda mrefu kati ya serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) kudai maslahi zaidi kwa wafanyakazi na kuitaka serikali kutekeleza baadhi ya ahadi zake za kuboresha maisha ya wafanyakazi. TUCTA imeandaa maandamano ya nchi nzima Julai 5 na kutamka kuwa isingemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.

DAR ES SALAAM, Aprili 26 (IPS) - 
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya alisema mishahara ya wafanyakazi wa umma ingetangazwa baadaye.

Katika tamko lake hilo la Aprili 20, 2010, waziri Kapuya alisema kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi wa migodini kitakuwa shilingi 350,000, viwandani shilingi 150,000, wafanyakazi wa mahotelini shilingi 80,000, mashambani shilingi 65,000 na majumbani shilingi 65,000.

Hatua ya waziri Kapuya ni nzuri kwani hali ya maisha imepanda ikilinganishwa na kima cha chini cha mishahara kinachotolewa sasa, siyo tu katika sekta binafsi, lakini pia kwa watumishi wa umma.

Lakini swali la kujiuliza, je ongezeko hilo la mishahara ni kwa faida ya nani?

Nakumbuka mwaka 2007 serikali ilitangaza kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi na watumishi wa umma.

Lakini je, tunaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani kupanda kwa mishahara wakati huo ambako kulitangazwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari kumeweza kuboresha maisha ya Watanzania?

Nikiwa ni mmoja wa Watanzania niliyekuwa nafuatilia kwa karibu kupandishwa kwa mishahara, niligundua kuwa siyo sekta binafsi nyingi ambazo ziliweza kupandisha mishahara hiyo.

Pili, sekta binafsi ambazo ziliweza kupandisha mishahara ziliweza pia kuongeza bei ya huduma au bidhaa zao nyingine mara mbili. Mfano, nilikuwa na mdogo wangu ambaye alikuwa akisoma shule ya sekondari wakati ule, ambapo nilikuwa nikilipa shilingi 500,000 lakini baada ya kuongezwa kwa kima cha chini, ilibidi shule ile kuongeza ada hadi shilingi 950,000.

Hata hivyo, mimi ambaye nilikuwa nafanya kazi kwenye NGO mshahara wangu haukuweza kuongezwa kutokana na mifumo ya NGOs ambayo hutegemea wafadhili. Siyo rahisi kwa NGO kuwashawishi wafadhili kuweza kuongeza mshahara tofauti na kiasi ambacho kinaonyeshwa kwenye mpango mkakati wa shirika.

Vile vile katika sekta ya utengengenezaji bidhaa za viwandani, nakumbuka, wahusika walipinga ongezeko hilo la mishahara kwa kudai haiendani na uwezo wao wa kuzalisha na kiasi ambacho wanaingiza kama faida. Walitishia kupunguza wafanyakazi na hivyo kuchochea baadhi ya migomo. Lakini hatimaye walipokabiliwa na mkono wa serikali, kazi yao ilikuwa rahisi, kuongeza bei ya bidhaa kwa walaji.

Sasa nimekuwa siku zote nikijiuliza, kupanda kwa kima cha chini cha mishahara hasa kwa sekta binafsi ni kwa manufaa ya nani? Najiuliza swali hili kwasababu kama wanaoongezewa mishahara ni wachache lakini wanaoumia ni wengi, kuna mantiki gani serikali kwa mbwembwe zote kutangaza ongezeko la mishahara kwa asilimia 100%? Nadhani serikali ingetumia njia nyingine ya kuboresha maisha ya wananchi wake zaidi ya kutangaza mishahara juu kwa asilimia 100% bila kuweka mikakati ya kuiwezesha mishahara hiyo kuwa kichochea cha kuboresha maisha ya Watanzania. (END/2010)

No comments:

Post a Comment