DONALD Trump aliyeshinda uchaguzi wa Marekani uliofanyika Novemba 8 mwaka jana, leo anaapishwa huku watu wengi kuanzia Marekani kwenyewe na nje ya taifa hilo kubwa duniani wakiwa na mtazamo na maoni tofauti. Kuapishwa kwa Trump kuwa rais wa 45 wa nchi hiyo, kunahitimisha miaka minane ya utawala wa rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Barack Obama.
Kinachosababisha kuapishwa kwa Trump kuwe gumzo duniani kote kunatokana na kauli zake tata alizokuwa akizitoa katika kipindi cha kampeni na hata baada ya kuchaguliwa kiti cha urais kupitia chama cha Republican na kumshinda aliyekuwa mpinzani wake mkubwa, Hillary Clinton wa Democrat.
Kuna wanaoamini kwamba baadhi ya aliyokuwa akiyasema wakati wa kampeni, yalikuwa ni maneno ya majukwaani pekee, lakini kuna wanaona kuwa anaweza kufanyia kazi kauli zake zilizoonekana tata kwa vitendo.
Kauli wakati wa kampeni Baadhi ya kauli tata za Trump wakati wa kampeni ni pamoja na azma yake ya kutaka Waislamu wasiruhusiwe kuingia Marekani.
Kadhalika, alisema atajenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ili kuzuia wahamiaji haramu kutoka nchi hiyo kuingia Marekani na kwamba atailazimisha Mexico kuugharimia.
Msimamo huu uliwashitua wengi kiasi cha Bunge la Uingereza kuketi na kufikiria kumzuia pia Donald Trump kuingia nchini humo. Hata hivyo, wabunge hao hawakupiga kura kutekeleza azma hiyo.
Sambamba na hilo, wakati wa kampeni mwaka jana, Trump aliahidi pia kuwarejesha kwa nguvu watu wanaokadiriwa kufika milioni 11 ambao walihamiaji nchini Marekani kwa njia zisizo za kisheria. Kadhalika alisema angewarejesha makwao wahamiaji kutoka Syria wanaotafuta hifadhi Marekani.
Amekuwa akibeza juhudi zinazofanywa duniani kote kuhusu changamoto za kudhibiti uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa. Amekuwa haamini kama binadamu amechangia mabadiliko ya tabianchi na anataka Marekani ijitoe katika Mkataba wa Paris.
Trump anaelezwa kwamba anaweza kuudhoofisha Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) kutokana na kutaka Marekani isitoe michango mikubwa katika umoja huo.
Rais huyo mpya ambaye aliahidi kuirejeshea Marekani 'hadhi yake' alisema Uchina inafaa kuchukuliwa hatua kali katika masuala kadha ili kuhakikisha usawa wa kibiashara unakuwepo kati yake na Marekani.
Baada ya kampeni Wamarekani wengi hawakufurahishwa na salamu za Trump za mwaka mpya ambazo alizitumia kupitia akaunti yake ya Twitter huku akiendelea kuwananga maadui wake wa kisiasa.
Aliandika: "Heri ya mwaka mpya kwa wote, ikiwa ni pamoja na maadui zangu na wale ambao walinipiga vita lakini nikawashinda vibaya na sasa hawajui la kufanya..."
Na kabla ya hapo, aliendelea kumchimba Rais anayemaliza muda wake, Obama, kwamba ingawa alijitahidi kumpigania Hillary Clinton na kukesha katika majimbo muhimu lakini aligonga mwamba! Donald Trump alidhihirisha kufurahia kumong'onyoka kwa Umoja wa Ulaya pale alipowamwagia sifa Waingereza waliopiga kura ya kutaka kujiondoa katika umoja huo.
Kama hilo halitoshi akazidi kuandika kwamba anaamini kwamba nchi zingine zitaunga mkono uamuzi huo.
Kauli hizi hazikuzifurahisha nchi ambazo bado ziko kwenye umoja huo, hususani Ujerumani.
Trump pia aliuponda Umoja wa Mataifa kupitia akaunti yake ya Twitter pale aliposema umekuwa kama baraza la watu kukusanyika na kupiga porojo. Hii ilikuwa ni baada ya jaribio lake la kupinga azimio lililokemea mpango wa Israel kuendelea kujenga makazi yao katika ardhi ya Wapalestina kufeli.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa Israel inakiuka sheria za kimataifa kwa kujenga katika ardhi ya Wapalestina.
Azimio hilo lilipitishwa huku Trump akitoa onyo kwamba mambo yatakuwa tofauti wakati atakaposhika rasmi hatamu za uongozi wa Marekani kuanzia leo.
Mbali na China, Trump pia aliitaja Singapore na India, kama nchi za bara Asia 'zinazoiba' nafasi za kazi kutoka Marekani. Hata hivyo India ilipongeza ushindi wake na kumkaribisha 'nyumbani'.
Trump na Afrika
Kuhusu Afrika, taarifa zilizopo zinaonesha kwamba Rais huyu mpya wa Marekani hajaliongelea kwa wema bara hilo.
Moja ya nukuu zake zilizosambaa zinaonesha kejeli kwa waafrika na viongozi wake kwamba ni wavivu, wezi na kwamba wanastahili kutawaliwa tena. Sera za Obama Baadhi ya sera za Obama alizotangaza kuachana nazo ni pamoja na ndoa za jinsia moja.
Alisema wakati wa mahojiano kuwa anapinga ndoa za jinsia moja licha ya kudai kuwa alishawahi kushudhuria ndoa ya aina hiyo. Lingine aliloahidi kulipiga vita akiingia madarakani ni ruhusa ya utoaji mimba isipokuwa kwa zilizopatikana kwa njia za ubakaji.
Kadhalika, alisema 'ataupiga chini' mfumo wa afya bima ya afya kwa watu wenye kipato cha chini unaojulikana kama Obamacare.
Wakosoaji wa Trump Wakosoaji wake wanamwelezea kuwa ni mbaguzi na mfitini na wapo wenye wasiwasi kwamba anaweza kuitumbukiza dunia kwenye janga kubwa.
Alikotokea Trump
Rais huyu mpya wa Marekani kuanzia leo ni mfanyabiashara tajiri anayemiliki majumba mengi, na aliyewahi kuwa mtangazaji wa kipindi cha maisha ya uhalisia kwenye luninga.
Alikuwa mtu anayeangazia sana ushindi katika maisha yake na alisema ni lazima afanikiwe katika kupata tuzo kuu duniani, yaani kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Trump alipita vizingiti vingi tangu mwanzo wa kampeni zake za kuwania urais zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Ni watu wachache walikuwa na fikra kuwa angeweza kuwania urais. Trump ambaye hakuwa mwanasiasa huko nyuma, walifikiri hangepata umaarufu lakini akaupata.
Wakasema hangeweza kushinda mchujo wowote lakini akafanya hivyo. Wakasema hangeweza kushinda uteuzi wa Republican lakini akathibitisha kwamba fikra zao si sahihi. Trump alimdhalilisha John McCain.
Akaanza ugomvi na mtangazaji wa kituo cha Fox News, Megyn Kelly.
Aliomba msamaha shingo upande wakati kanda moja ya video ilipotolewa akijigamba jinsi alivyowadhalilisha kimapenzi wanawake.
Alipambana na pingamizi ndani ya chama chake na kushinda zote. Trump alipambana vikali na washindani wake aliokuwa nao kwenye mchujo, akina Marco Rubio, Ted Cruz, Chris Christie na Ben Carson. Donald Trump alizaliwa 14 Juni 1946, katika Manispaa ya Queens katika jiji la New York.
Ni mmoja wa watoto watano wa Mary Anne (nee MacLeod) na Fred Trump, ambao walifunga ndoa mwaka 1936. Kaka yake mkubwa, Fred Jr., alifariki dunia mwaka 1981 akiwa na umri wa miaka 43.
Donald ni mtoto wa tano kati ya watoto sita. Baba yake, Fred, alikuwa tajiri aliyemilki majumba.
Mama yake alikuwa mhamiaji kutoka Scotland, alizaliwa katika Kisiwa cha Lewis, pwani ya magharibi ya Scotland, na mababu wa Trump upande wa baba walikuwa wahamiaji kutoka Ujerumani.
Babu yake, Frederick Trump alihamia nchini Marekani mwaka 1885, na kuwa raia wa Marekani mwaka 1892.
Tangu utotoni, Trump alikuwa mtundu na wazazi wake walimpeleka shule ya msingi iliyofadhiliwa na jeshi mjini New York.
Baadaye alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania, kitivo cha elimu ya biashara mwaka wa 1968 na kupata Shahada ya Sayansi katika Uchumi.
Awali alihudhuria mafunzo katika Chuo Kikuu cha Fordham katika eneo la Bronx kwa miaka miwili, kabla ya kuhamia Shule ya Wharton ya Chuo Kikuu cha Pennsylvania.
Alifanya kazi katika kampuni ya babake, Elizabeth Trump & Son, wakati akisoma katika Shule ya Wharton ya Chuo Kikuu cha Pennsylvania, na mwaka 1968, alijiunga rasmi na kampuni hiyo, ambayo babake aliendesha biashara ya kuuza nyumba kwa raia wa kipato cha kati, viungani mwa New York.
Hata hivyo, Donald Trump alikuwa na ndoto ya kufanya biashara nje ya makazi ya Queens na Brooklyn.
Donald alipewa udhibiti wa kampuni hiyo mwaka 1971, na kuiita The Trump Organization.
Trump anabaki kuwa mfano mkubwa katika sekta ya majengo na mali isiyohamishika nchini Marekani na mtu maarufu kwenye vyombo vya habari.
Aliwekeza katika biashara kubwa ya ujenzi na kuweza kujenga mojawapo ya majengo ya kifahari zaidi nchini Marekani. Alifanikiwa kutokana na sera ya kiuchumi iliyowekwa na utawala wa Reagan miaka wa 1980.
Aliwahi kuiambia tume ya uchaguzi kwamba utajiri wake unafikia dola bilioni 10.
Hata hivyo jarida la Forbes limenadi kwamba utajiri wa Trump haufikii juu ya dola bilioni 4.5. Lakini unapotembea barabara kuu za Manhattan, kampuni ya Trump imeweka mabawa yake kwa majumba ya kifahari yaliyofuatana.
Yapo mahoteli, viwanja vya mchezo wa gofu, makazi ya kifahari, majumba ya kamari kutoka Carlifonia hadi Mumbai nembo yake ikiwa ni Trump.
Ameandika Riwaya kadhaa kuhusu biashara, huku umaarufu wake uking'aa zaidi katika makala yanayoelezea maisha halisi, “The Apprentice,” katika televisheni ya NBC.
Hata hivyo, alitupwa nje ya makala hayo baada ya kutoa kauli zilizowakera raia wa Mexico.
Licha ya kufanikiwa katika biashara, mara nne kati ya mwaka 1991 na 2009, miradi yake ya hoteli na majumba ya kamari ilitangazwa kufilisika.
Ndoa zake mbili zimevunjika.
Mwaka 1977, Trump alifunga ndoa na Ivana Zelnickova, mwenyeji wa Jamhuri ya Czech, na kuzaa naye watoto watatu: Donald Jr. (amezaliwa 31 Desemba 1977), Ivanka (aliyezaliwa 30 Oktoba, 1981), na Eric (amezaliwa Januari 6, 1984).
Waliachana mwaka 1992.
Na mwaka 1993, alimuoa Marla Maples na kuzaa naye mtoto mmoja, Tiffany (13 Oktoba 1993). Wakatalikiana Juni 8, 1999. Aprili 26, 2004, alimchumbia Melania Knauss, mwenyeji wa Slovenia.
Trump na Melania walioana Januari 22, 2005, katika Kanisa la Sea Episcopal katika Bethesda, kwenye kisiwa cha Palm Beach, Florida. Melania alijifungua mtoto wa kiume aitwaye Barron William Trump, mtoto wa tano wa Trump, Machi 20, 2006.
No comments:
Post a Comment